Skip to main content

MALARIA

UFAHAMU ZAIDI UGONJWA WA MALARIA
By DALUS

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyojulikana kama Plasmodium.

Vimelea hivi huenezwa na mbu jike aina ya anofelesi (anopheles).
Lakini watu wengi huelewa kwamba malaria husababishwa na mbu. Mbu huyu husaidia katika usambazaji tuu wa vimelea husika.

Aina ya vimelea ambavyo humdhuru binadamu kati ya vimelea vingi vya Plasmodium ni:
Plasmodium falciparum - Wadudu hawa ndio hatari kushinda wengine kwa sababu wanashambulia seli zilizokomaa na ambazo ni changa.

Hupatikana sana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara.
Asilimia 75 ya wagonjwa wote wa malaria barani Afrika husababishwa na vimelea hivi.

Mwaka 2006, kati ya watu milioni 247 duniani waliougua malaria, asilimia 91 walisababishwa na vimelea hivi (Afrika 98%) na kusababisha vifo kwa asilimia 90 mwaka huo huo barani Afrika.

Plasmodium malariae - Pia hupatikana katika nchi zilizopo katika jangwa la sahara, Asia ya Mashariki, Indonesia na katika visiwa vya magharibi mwa Pacific.

Kati vya vimelea vyote vya malaria, plasmodium malariae ndio huonekana kwa uchache zaidi.
Plasmodium ovale - Hupatikana Afrika Magharibi, Ufilipino, Mashariki mwa Indonesia, Papua New Guinea, Cambodia, Bangladesh, India, Thailand na Vietnam. Plasmodium vivax -
Huonekana katika bara la Marekani, Latin Amerika na baadhi ya sehemu za bara la Afrika.

Plasmodium knowlesi - Hupatikana katika bara la Asia ya mashariki katika nchi za Bormeo, Myanmar, Malaysia, Ufilipino, Singapore na Thailand. Haipatikani katika bara la Afrika.

Mzunguko wa maisha ya vimelea vya malaria Mwenyeji wa msingi ya vimelea vya malaria ni mbu aina ya anopheles wa kike, ambae pia ni msambazaji, na binadamu ni mwenyeji wa kati. 

  Mbu anapokuwa anajipatia chakula kwa kunywa damu kwa kuuma binadamu mwenye maambukizi ya vimelea vya malaria, ndio mzunguko wa kwanza huanza, ambapo gametocyte za vimelea vya plasmodium hugawanyika ndani ya mbu na  kutengeneza gametocyte za kike na za kiume na baada ya hapo gametocyte hizo za kike na za kiume, hujiunga ndani ya mfumo wa chakula wa mbu na kutengeneza Ookinete ambayo hupenyeza kwenye kuta za mfumo wa chakula na kutengeneza Oocyst nje ya ukuta wa mfumo wa chakula, na hapo hupasuka na kutengeneza Sporozoites na kuhamia kwenye tezi za mate za mbu, na kuwa tayari kuambukiza binadamu mwengine pindi mbu anapojitafutia chakula.

Kwa mbu jike damu ndio lishe yake wakati dume lishe yake ni nekta ya mimea, hivyo mbu dume hasambazi ugonjwa huu.

Na mbu jike aina ya anopheles hupenda kujipatia lishe kipindi cha usiku. Maambukizi ya malaria yanaweza kupatikana kwa kuongezewa damu ingawa ni nadra sana.

Nini hutukea mwilini baada ya vimelea hivi kuingia mwilini Kwa Binadamu pindi anapong’atwa na mbu hupata maambukizi kupitia mate ya mbu, na vimelea vya plasmodium kwenye hatua ya sporozoites huingia kwenye damu na kuelekea kwenye seli za  ini ambapo hutengeneza schizonts na baadae schizonts hupasuka na kuachia merozoites kuelekea kwenye damu,merozoites wanaingia kwenye seli nyekundu za damu na kuzaliana wanapojaa seli inapsuka na kuachia merozoites wengi zaidi ambao wanaingia kwenye seli nyekundu nyingine za damu. kipindi seli zinapasuka ndo hapo mtu anapata homa.

Baada ya hapa huwa kuna hatua mbili tofauti zinazofuata,hatua ya kwanza ni mature trophozoites na kutengeneza schizont nyingine kwenye damu na vilevile schizont hii hupasuka na kutoa immature trophozoites na kuendelea kujirudia tena hatua hii.
Hatua nyingine ni gametocyte ambayo hubebwa na mbu.

Dalili za malaria zinategemea mtu na mtu kutokana na nguvu ya kinga yake. Hata hivyo dalili zinazowapata wagonjwa wa malaria zinatokana na hatua ya ugonjwa aliyonayo mtu aliyeambukizwa. Kuna aina mbili za malaria:

1. Malaria ya kawaida, isiyokuwa kali au sugu kitaalamu inaitwa “Uncomplicated Malaria”. Hii inakuwa haijasababisha madhara makuwa katika mwili.

2. Malaria sugu, kitaalamu “Complicated Malaria”.
Hii imeishasababisha madhara kama kuharibu viungo muhimu mwilini kama, ubongo (kupoteza fahamu – cerebral coma), figo (figo kufeli-renal failure), ini (ini kufeli -liver failure), moyo (moyo kufeli – heart failure), mapafu (mapafu kufeli – pulmonary failure), upungufu wa sukari mwilini (hypoglycaemia).
Na pia kuwa na vimelea vingi (hyperparasitaemia).

Dalili za malaria isiyo kali
1. Homa ikiambatana na maumivu ya kichwa
2. Maumivu ya mwili
3. Tumbo kuuma na kuharisha
4. Kichefuchefu na kutapika
5. Kizunguzungu
6. Kutokwa jasho
7. Kutetemeka
8. Kifua kuuma
9. Kukosa hamu ya kula

Dalili za malaria kali
1. Mabadiliko katika mwenendo na tabia (kuchanganyikiwa)
2. Uchovu mkubwa kupita kiasi (mgonjwa hawezi kukaa au kusimama)
3. Upungufu mkubwa wa damu (mgonjwa husikia kizunguzungu sana)
4. Kupoteza fahamu
5. Kupumua kwa shida
6. Degedege/mtukutiko mwili (Kwa watoto wadogo)

7. Kutapika kila kitu, kushindwa kunywa au kunyonya kwa watoto

8. Mzunguko hafifu wa damu, kutokwa damu isiyo ganda kwa urahisi

9. Figo kushindwa kufanya kazi na kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi/kahawia. Kumbuka: Malaria hushambulia zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano

(5), wanawake wajawazito na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi. Hii ni kutokana na kinga zao za mwili huwa chini. Hizi dalili pia hutokea katika magonjwa yanayoambukizwa na bakteria, kwa mfano:

Homa inaweza kuwa dalili ya UTI, Pneumonia, Typhoid, n.k Kukohoa kunaweza kuwa sababu ya maambukizi katika mapafu mfano pneumonia, kifua kikuu n.k Kutapika na kuharisha inaweza kuwa dalili za magonjwa ya maambukizi ya tumbo pia.

Hivyo ni vema ukipata dalili hizi usichukue dawa bila kupata uchunguzi wa kitaalamu na pia ushauri kutoka kwa madaktari. Unapopata dalili hizi wahi hospitali ili wataalamu wakuchunguze na kujua ni ugonjwa gani ulionao.

Matibabu ya Malaria Kwa malaria isiyosugu/isiyokali, dawa inayopendekezwa kwa sasa kama tiba ya kwanza ni dawa ya Mseto (ALU), pia gonjwa anatumia dawa akiwa nyumbani kwake.

Kutokana na dalili za mgonjwa huyu, inawezekana anaweza kula na kunywa vizuri na dalili nyingine pia sio za kushtua sana ndio maana mgonjwa hupewa vidonge na ushauri wa mlo na vitu vya kuepuka akiwa anatumia dawa za malaria, hususani bidhaa za pombe.  Kwa wajawazito wenye ujauzito wenye umri wa chini ya miezi mitatu hawaruhusiwi kutumia ALU, wanatibiwa kwa kutumia quinine.

Kwa malaria sugu, matibabu yanayopendekezwa kama tiba kwa mgonjwa ni dawa ya Quinine kwa njia ya dripu na sindano zinazojulikana kama Artesunate na Artemether.

Pia mgonjwa anapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Mgonjwa analazwa hospitalini hadi anapopata nafuu na kuweza kula mwenyewe.

Wagonjwa wengi wenye malaria kali au sugu, kutokana na hali yao ya kupoteza fahamu, kutapika kila kitu na kushindwa kula, pamoja na dalili zingine kama zilivyoorodheshwa hapo juu, ni vyema walazwe ili wapewe huduma stahiki.

Jinsi ya kujikinga na Malaria Malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo nchini Tanzania. Ila ni ugonjwa ambao vilevile kwa maamuzi na bidii za binadamu ugonjwa huu unaweza kukwepeka. Hivyo basi, zifuatazo ni namna mbalimbali za kujikinga na malaria:

1. Kutumia chandarua kilicho wekwa dawa ya kuua mbu. Kutumia tu chandarua haitoshi. Ni muhimu kulala kwenye chandarua kilicho na dawa.

Chandarua nyingi zinazouzwa madukani kwa muda huu zimeshawekwa dawa tayari, lakini unashauriwa kuuliza na kuwa na uhakika kuwa chandarua unachonunua kimewekwa dawa.

2. Kuweka mazingira safi kwa kufukia madimbwi na mashimo yasababishayo maji kutuama. Maji yanayotuwama huzalisha sana mbu.

Mayai ya mbu hupendelea maeneo yenye majimaji lakini yasiyokuwa na kusogea (yaliyotuama), mfano madimbwi ya maji ya mvua yaliyokaa muda mrefu bila kukauka, unyevunyevu vichakani na kwenye nyasi ndefu, makopo yenye uwazi yaliyotelekezwa na kujaa maji ndani yake, magari mabovu yaliyonyeshewa mvua na kukusanya maji ndani, mabwawa madogomadogo kama ya kufugia samaki n.k.

Hivyo ni vyema kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kuchoma au kusafisha makopokopo na magaloni na pia kuondoa magari mabovu na chochote kinachoweza kukusanya maji kwa muda mrefu kwa eneo lote linalozunguka nyumba yako.
Ukifanya hivi utakuwa umesababisha hatua muhimu ya kisababishi cha malaria (mbu) asizaliwe.

3. Kuteketeza mazalia ya mbu kwa kunyunyuzia dawa ya DDT.
Baada ya kufanikisha namba mbili hapo juu, na kuna sehemu ambazo mazalia ya mbu yanaweza kutokea na hakuna jinsi ya kuepuka maji haya yaliyotuama inashauriwa kunyunyuzia dawa ya DDT.

Dawa hii ni sumu ambayo pia inaweza ikamdhuru binadamu. Hivyo shughuli ya kunyunyizia dawa hii hufanywa na wataalamu wa afya na mazingira.

4. Kufukuza na kuzuia kung`atwa na mbu. Ni ukweli kwamba pamoja na juhudi zote hapo juu bado kuna uwezekano wa kung`atwa nambu kwani tupo kwenye eneo la tropiki ambalo ndio makazi yao.

Hivyo basi njia nyingine za ziada zinahitajika kujikinga using`atwe na mbu waliofanikiwa kuzaliwa. • Kuua mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba.

Kuna baadhi ya kampuni wanafanya kazi ya kuua vimelea (fumigation) maeneo mbalimbali. •
Kufukuza mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba (Ifahamike kuwa kuna dawa ambazo zina uwezo wa kufukuza pekee na kuna ambazo zinaua kabisa hivyo unavyonunua dawa dukani elewa unanunua dawa ya aina gani ili uitumie kama inavyoelekezwa) • Kuzuia mbu – Dawa za kupaka.

Kwa wakati ambao haupo nyumbani inawezekana ukawepo kwenye sehemu yenye mbu, mfano baa, mpirani au hata kazini katika ule muda ambao mbu hung`ata, ni vyema ukajikinga nao kwa kujipaka dawa mbalimbali za kuwafukuza au kuwaua mbu pale wanapokukaribia au kuanza kukung`ata.

Dawa hizi zinatoa harufu ambayosio rafiki kwa mbu hawa au zina uwezo wa kuwaua pindi wanapoanza kukuchoma. 5. Kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa kina mama wajawazito ni muhimu.

Wajawazito wana hatari kubwa zaidi ya kung`atwa na mbu kutokana na mabadiliko yao ya kimwili, mfano joto la mwili kuongezeka, hivyo mbu huweza kuwafikia kwa urahisi zaidi. Inapendekezwa na wizara ya afya kwamba wanawake wajawazito watumie dawa ya malaria aina ya “SP” kabla ya kujifungua.
Hii itawasaidia kama kinga dhidi ya malaria kwao na kwa watoto wao tumboni.

Dozi ya dawa hizi hutolewa katika vituo vya afya vinavyo toa huduma kwa mama na mtoto. 6. Ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za malaria kwa wagonjwa.

Kuzingatia dozi sahihi inaweza ikawa kinga kwa maambukizi mengine yanayokuja.
Vilevile kutokumaliza dozi kunamaanisha kuviacha baadhi ya vimelea mwilini ambavyo havikufa tayari mpaka kipindi ulipoacha dozi. 7.

Usitumie dawa bila kumuona daktari kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaongeza usugu wa dawa mwilini mwako bila sababu ya msingi na pia unahatarisha maisha yako.

Usugu wa dawa za malaria ni hatari na inamaanisha ukipata malaria na vimelea ulivyonavyo vimeshakuwa sugu kwa dawa zilizopo za malaria, maisha yako yanakuwa hatarini kwani madaktari watashindwa kukutibu.
Madhara ya ugonjwa malaria Malaria ya kichwa (cerebral malaria)
Matatizo ya kupumua (pulmonary edema)

Viungo kushindwa kufanya kazi (organ failure)
Upungufu wa damu
Upungufu wa sukari mwilini (hypoglycemia) Shinikizo la chini la damu (hypotension)

Muhimu Malaria ni ugonjwa hatari unaoua kwa haraka hivyo pindi unapohisi una dalili za malaria kama zilivyoorodheshwa hapo awali, wahi katika kituo cha kutoa huduma za afya kilichokaribu na wewe ili upatiwe uchunguzi na kupata tiba sahihi.

Comments

Popular posts from this blog

MTOTO KATIKA UKUAJI

HATUA MUHIMU ZA UKUAJI WA MTOTO KISAIKOLOJIA Dr. DALUS Mtoto anapitia mabadiliko mbali mbali ya kimwili,kiakili na kisaikolojia pindi anapokua anakuwa hadi kuwa mtu mzima. leo nitakuelezea hatua za ukuaji wa mtoto kisaikolojia muhimu sana katika malezi yake. hatua hizo ni kama ifatavyo 1.ORAL STAGE Mtoto anakua katika stage hii anapokuwa na umri wa,mwezi mmoja hadi mwaka mmoja.   Sasa kwa kipindi hiki erogenous zone ya mtoto inakua mdomoni, raha ya mtoto inakua kitu chochote kinachoingia mdomoni ndo maaana kipindi hiki mtoto kila kitu anachoshika anapeleka mdomoni . Hiki ndo kipindi cha kujenga strong bond kwa mtoto na mama pale mtoto anapokuwa ananyonya inamjenga kumthamini mama kuliko mtu yyte Kipindi hiki inabdi kuwa makini na vitu kama shanga,sarafu nk ambavyo akiweka mdomoni vnaweza kumkaba Hapa kama mzazi ana tabia ya kula kucha ndo kipindi mtoto nae anajifunza na kua hvo anapokua 2.ANAL STAGE Stage hii inaanza umri wa mwaka 1 hadi miaka mi 3 Hapa mtoto raha yake ni ...

BIMA YA AFYA NA FAIDA ZAKE

BIMA YA AFYA NA FAIDA ZAKE By Dalus Bima ya afya ni nini? Bima ya afya ni mfumo wa kujiunga kwa hiari ama kwa lazima unaomhakikishia mwanachama kugharamiwa gharama zozote zinazojitokeza katika kupata huduma za kiafya zikiwemo kumwona daktari, kufanya vipimo pamoja na kupata matibabu na dawa kwa mwanachama husika. Bima ya afya ni kama mkataba unaoingiwa na anayetaka huduma pamoja na mtoa huduma kwa kupitia mifuko au taasisi inayowaunganisha mtoa huduma pamoja na mhitaji wa huduma husika. Mara nyingi Bima ya afya hujumuishwa kwenye makato anayoyatoa mwajiri kwa waajiriwa wake katika kufanya malipo. Pia zipo bima zinazowahusu watu binafsi, wazee na wasiojiweza, wajawazito na wengine wenye mahitaji maalumu bila kusahau wanafunzi kipindi cha masomo yao. Mara nyingi wanachama huchagua taasisi ama mifuko inayotoa bima hizi kulingana na aina, viwango na mipaka (coverage) ya Taasisi/Bima hizo. Ni ukweli uliowazi kuwa kila mfuko huweza kutofautiana na mingine katika huduma inazozitoa kwa...

FAIDA ZA NDIZI MWILINI

FAIDA ZA NDIZI MWILINI Ndizi mbivu ni tunda linalotumika sana kama mlo sehemu mbalimbali duniani. Ni tunda ambalo ni tamu na lenye virutubisho mbalimbali na muhimu kwa mwili. Baadhi ya faida za ndizi kiafya ni kusaidia moyo kufanya kazi vizuri, kupunguza uwezekano wa kupata saratani na pumu. Ndizi ni chanzo kizuri cha madini ya Potasiamu. VIRUTUBISHO VILIVYOMO KWENYE NDIZI Ndizi ya wastani ina uzito wa kama gramu 126O. Ina nishati kiasi cha kalori 110, gramu 30 za wanga na gramu 1 ya protini. Ndizi hazina fati, lehemu (cholesterol) au madini ya Sodiamu. Ndizi zina virutubisho  vifuatavyo; Vitamini B6 – 0.5 mg Manganizi- 0.3 mg Vitamini C – 9 mg Potasiamu – 450 mg Kambakamba- 3g Protini – 1 g Magneziamu – 34 mg Madini ya Foliki- 25.0 mcg Riboflavin – 0.1 mg Niacin – 0.8 mg Vitamini A – 81 IU Madini ya chuma – 0.3 mg FAIDA ZA NDIZI KIAFYA Kushusha Shinikizo la Damu Ndizi zina madini ya Potasiamu kwa wingi amb...